Robert akiwa kwenye gari lake alianza kulia, akashindwa hata kuendesha akaamua kusimama kando ya Barabara akiwa anabubujikwa na machozi.
Machozi yakawa yanamtiririka Robert huku akizidi kulia kwa uchungu mkubwa, jua lilikua likiwaka huku Watu wakiendelea na shughuli zao lakini kwa Robert ilikua tofauti sana, alijikuta yupo kwenye kisa chenye utata sana.
Alikua amevalia Suti nyeusi, kiatu cheusi lakini sura yake hofu na hali ya majuto ilikua imetanda sana. Akajikuta akipiga usukani kutokana na hali aliyokuwa nayo, akageuka nyuma ya gari.
Kulikuwa na Mwili wa Mtu uliokuwa ukivuja damu, mwili huo hapana shaka ulikuwa ni wa kike kwani ulikuwa na vazi la Shela.
Robert akaliondoa gari pale kando ya ile barabara, sasa akawa barabarani kuelekea alipokusudia huku ile hali ya kulia ikiwa imekata. Simu yake ilikua ikiita mno lakini hakutaka kuipokea, Alipofika mbele akaachana na barabara kuu akaingia barabara ya vumbi ambayo ilikua ikielekea ufukweni.
Robert alipofika juu ya kilima akaongeza mwendo akalitumbukiza gari hilo ndani ya bahari na kuzua taharuki kwa Watu waliokuwa upande mwingine wa ufukwe, kelele na taharuki vikaamka pale Ufukweni, Watu wa uokozi wakawa tayari kwa ajili ya kuzama majini kulitoa gari hilo.
Kwa muda mfupi lile gari lilikuwa limezama ndani ya yale maji ya Bahari ambapo kwa upande ule kulikuwa na kina kirefu ambacho Watu walikuwa hawaendi kuogelea, Punde polisi wakaja pale huku Watu wakiendelea kupigiana simu kuwa kuna gari limezama ndani ya Bahari, kilikuwa ni kituko kwa kila aliyesikia, kila Mtu akataka kujua ilikuwaje.
Polisi wakazungusha utepe wao kuashiria kuwa eneo hilo halikuwa salama kwa wakati huo, ziliwachukua zaidi ya dakika 45 waogeleaji kuchopoa miili miwili. Moja ilikuwa ni ile ya kike na nyingine ilikua ni ya Robert, gari ya huduma ya kwanza ikaichukua miili ambapo yote ilikuwa tayari haina uhai.
Taarifa hii ikawa na mkanganyiko mkubwa kwa Watu walioisikia, haikuhitaji uchunguzi mkubwa sana kugundua kuwa walikuwa ni Wanandoa au watarajiwa, mwili wa Mwanamke ulikutwa na risasi shingoni.
“Ufanyike uchunguzi haraka sana kuhusu hili tukio” Akaagiza mkuu wa Upelelezi.
- ••••••••
Vilio vilikuwa vimetanda ndani ya kanisa moja lililopo katikati ya Jiji, tayari polisi walikuwa wamefika na kuukuta mwili mwingine uliokuwa umejeruhiwa kwa risasi, ulikuwa ni mwili wa Mwanaume mmoja ambaye alitambulika kama Bosco, naye alikuwa amevalia suti.
Polisi wenyewe walipigwa na butwaa kwa jinsi hali ya vilio ilivyokua imetanda ndani ya kanisa hilo kubwa na lenye hadhi, Watu wengi walikuwa wakisimuliana kilichotokea hapo.
Mama mmoja alikua akilia kwa uchungu huku akiutikisa mwili wa Bosco uliokuwa umeloa damu, shati jeupe alilovaa lilikua limetapakaa damu mno.
“Mwanangu mimi! Eeeh Mungu mtihani gani huu umenipa mimi leo tena mbele ya Kanisa” Sauti ya kilio iliyotoka kwa kwikwi ilimtoka Mama huyo, mmoja wa Askari akapata shahuku ya kumfuata huyo Mama.
“Pole Mama!” Akasema huku akiwaambia watu wa Huduma ya kwanza wauchukue ule mwili kwa ajili ya taratibu za kiupelelezi zaidi.
Lilikua ni pigo lililoamsha kilio chake, Mwili wa Bosco ulikuwa ukiwekwa kwenye gari maalum kwa ajili ya kuupeleka Hospitali, mkononi Askari huyo aliyejitambulisha kama Inspekta Zola alikua ameshikilia karatasi yenye majina ya Watu waliopoteza Maisha kwenye kisa kile cha kutisha. Jina la Robert lilikua la kwanza, la pili ni Sandra na la tatu ni Bosco. Akajiuliza Watu wale walikua kwenye kisa gani kilichopelekea vifo vyao.
Akamfwata Mtu mmoja aliyekua amekaa kando, alikua amejitenga sana na wengine. Kupitia jicho la Kipelelezi Inspekta Zola akagundua jambo, alipomfikia akamuuliza
“Nini kimetokea?” Ilikua ni kama vile ameamshwa kutoka kifo, akajikuta akishtuka sana. Naam! alikuwa ni Mdada mwenye sura ya upole, mweupe mwembamba, kwa jinsi alivyovaa ilikua rahisi kutambua kuwa hakua miongoni mwa Watu waliofika kwa ajili ya ile shughuli pale Kanisani.
“Unaitwa nani?”
“Judith!!”
“Huonekani kama mmoja wa Waalikwa hapa, kimekuleta nini?” Swali hili likaambatana na jicho kavu la kipelelezi
“Mimi?”
“Ndio wewe kwani naongea na nani?” Mdada akakaa kimya bila kujibu chochote huku akionesha kutetemeka, Yule Askari akamchukua Mdada kwa ajili ya mahojiano zaidi pamoja na baadhi ya Watu ambao walitambulika kama ndugu wa Bosco ambaye amefariki kwa kupigwa risasi.
Ilikua ni siku ya majonzi sana, vilio vilitanda hadi kituo cha polisi ambapo baada ya polisi kuwataka watulie ndipo vilio vilipokoma.
“Nini kimesababisha vifo vyao?” Aliuliza Inspekta Zola ambaye alikua makini, mbele yake kulikua na Ndugu zake Bosco na wengine ambao walijitambulisha kama ndugu wa Sandra, yule Mdada alikua amekaa pembeni akiwa katika hali ya hofu.
“Inatisha na kusikitisha Afande, marafiki walioshibana leo wanauwana” akaongea Mama yule ambaye alifahamika kama Ndiye Mama yake na Bosco, kilio kilianza tena ikabidi sasa Inspekta Zola amuondoe Huyo Mama kwasababu asingeliweza kuzungumza chochote zaidi ya kilio.
“Nini kimetokea?” akauliza tena Inspekta Zola akiwatazama walioko mbele yake, mmoja akatikisa kichwa ishara ya kuwa hajui hasa kilichosababisha vifo vya Watu watatu, Inspekta Zola akapata wazo la kumuuliza yule Mdada, akamuita
“Nini kimetokea?” Akamuuliza yule Mdada ambaye hata baada ya kuulizwa alikaa kimya kwa kitambo kidogo kabla ya kuanza kuzungumza.
Chozi likianza kumbubujika akajikuta akianza kuongea.
“Mapenzi! Najiuliza kwanini yameumbwa, kwanini yanatesa, yanafanya Watu wawe maadui, watu wapoteze furaha walizonazo! Ni mapenzi” Kila mmoja alikaa kimya baada ya huyo Mdada kuanza kuzungumza, Familia zote zilizopo pale polisi zilikaa kimya kumsikiliza Mtu ambaye hawakumfahamu.
“Huyu ni Muongo” Akadakia Dada Mmoja aliyekuwa akibubujikwa machozi
“Hebu subiri aongee alafu sisi tutapima maneno yake kama yamejaa ukweli au uwongo” akaongea Inspekta Zola
“Nawaomba polisi mufanye kazi yenu lakini sio kusikiliza maneno ya Mtu huyu, Mdogo wangu Sandra hakuwahi kuingia kwenye vita ya Mapenzi, anaongea Uwongo Mtupu…”
“Mpaka hapa tunapozungumza hakuna aliye hai ambaye anayeweza akatueleza kilichotokea, ni vema tukamsikiliza huyu Binti”
“Una maanisha nini? Mdogo wangu Robert amekufa?” akauliza kwa Mshituko kuhusu Robert ambaye mwili wake uliopolewa Baharini baada ya kulitosa gari lake ndani ya Bahari.
“Sandra na Robert wamekutwa wakiwa tayari wamekufa ndani ya maji, ndio maana nasema tukae kimya kumsikiliza ili kama kuna ukweli unazungumzwa basi ndio utatupa uelekeo wa kujua chanzo cha vifo hivi vya Kutisha” Akajibu Inspekta Zola, taarifa ikaamsha tena vilio
“Nilijua Robert atakuwa salama jamani”
“Nini kimetokea Robert Mwanangu…Nini Babaaa??”
“Bosco mlikuwa mnaficha nini kwenye maisha yenu wanangu?” Zilikuwa ni sauti zilizojaa vilio hadi Inspekta Zola akaamuru sasa watolewe nje ili afanye mahojiano na huyo Mdada ambaye alionesha kufahamu baadhi ya mambo!
“Judith sitaki uingie matatizoni, unaonekana sio mtu mbaya…sura yako inaonesha hujahusika kwenye jambo hili lakini unafahamu kitu..lisaidie jeshi la polisi, nini kimesababisha vifo hivi vya kutisha na ilikuwaje pale kanisani?” Chozi likaanza kumbubujika Judith akiwa anamtazama Inspekta Zola ambaye alikua makini kusikiliza atakacho kisema.
“Judith…unafahamu nini kuhusu Maisha ya Bosco, Sandra na Robert?” akauliza tena Inspekta Zola lakini bado Judith aliendelea kulia.
“Mapenzi yamefanyaje Judith? wewe ni sawa na binti yangu na huwa naumia sana kumuona Binti kama wewe ukiingia kwenye matatizo”
Judith akajifuta mchozi uliokua ukitiririka kwenye mashavu yake akavuta hewa kama Mtu mwenye mafua kisha akamkodolea macho Inspekta Zola
“Tupo mimi na wewe tu, tuongee kama Mtu na Baba yake Judith…Nini kimetokea?” Kauli hii ikamfanya Judith avute hewa, akajisikia uhuru fulani wa kuzungumza. Macho ya Inspekta Zola yaliyokomaa Kijasusi yakawa yana Mmulika Judith ndani ya Chumba kimoja cha mahojiano.
“Unawafahamu vipi hawa Watu?” aliuliza tena Inspekta zola tena bila kuchoka
Judith akanyanyua kinywa chake ili aanze kueleza kilichotokea, mara mlango ukafunguliwa akaingia Polisi mmoja aliyevalia sare za kipolisi, akapiga saluti kwa Inspekta Zola.
“Ripoti ya uchunguzi wa miili ya Marehemu wote Watatu” Akaongea polisi aliyeingia, akamkabidhi baasha Inspekta Zola, akaifungua ili asome ripoti hiyo.
Akazisoma ripoti zote lakini ripoti ya mwili wa Sandra ilimshangaza kidogo licha ya kukutwa kwa risasi sehemu ya shingo pia Mwili ulikutwa na tatuu ya jina la Bosco upande wa kulia wa paja lake lakini pia upande wa kushoto wa paja lake lilikutwa jina la Robert. Inspekta Zola akamtazama yule polisi kisha akarudisha macho yake kwa Judith, akawa na maswali mengi yaliyohitaji majibu ya haraka.
“Sandra alikua na mahusiano na Bosco na Robert kwa wakati mmoja?”
“Ndio”
“Je, Robert na Bosco walikua wakijuana kwenye penzi la Sandra?”
“Hapana”
“Walikua marafiki walioshibana sasa waliwezaje kuishi kwenye penzi la Mtu mmoja?” Akauliza Inspekta Zola, kisha akatazama saa yake tayari usiku ulikua umeingia.
“Afande utahakikisha anakua salama huyu binti hadi kesho asubuhi” akasema Inspekta Zola kisha akaondoka zake pale kituo cha polisi, Judith akachukuliwa kwa maelekezo maalum ya Inspekta Zola akapelekwa sehemu ili apumzike ndani ya kituo kile cha polisi.
- ••••••••
Nyumbani kwenye familia ya Robert bado vilio vilikua vimetawala kila mmoja akijiuliza Robert alikua amepatwa na nini hadi akawapiga risasi Sandra na Bosco, wote walishuhudia tukio hilo ndani ya kanisa. Ndugu walikua wakifika kwa ajili ya mazishi ya Robert, pia upande wa Bosco hali ilikua hivyo hivyo, pia kwa Sandra hali ikawa hivyo hivyo.
Hakuna aliyejua hasa sababu ya Marafiki hawa walioshibana kuangukia kwenye kivuli cha Umauti.
Baada ya kutoka kituo cha Polisi Inspekta Zola akaelekea nyumbani kwake, siku hii hakuwa katika hali ya kawaida bali kwenye tafakari nzito kuhusu kisa kile kizito ambacho kilikua mikononi mwake. Taarifa iliyopo kwenye meza yake ilikua ni Robert kumpiga risasi Bosco, kisha kumpiga risasi Sandra na kwenda kujitosa ndani ya Bahari.
Akiwa kwenye chumba chake maalum kwa ajili ya upelelezi akaanza kuvuta picha tofauti tofauti ambazo alikua akizifikiria lakini hakufanikiwa kupata picha halisi ya tukio lile, umri wake wa miaka 60 ulitosha kumwambia kuwa kisa kile kilikuwa na simulizi ya kusisimua ndani yake.
Akachukua karamu na karatasi akaandika ” ROMEO NA JULIET” kisha akafuta kwa kuamini kuwa visa hivyo ni tofauti, akamaliza kwenda kitandani na kujitupa, akajigalagaza hadi Usingizi ulipomchukua.
Asubuhi jua likiwa tayari limetoka akaamshwa na mlio wa simu yake ya mkononi iliyokua pembezoni mwa Kitanda chake. Akaamka na kuipokea, akajua kuwa siku ilikua imeanza. Akajiandaa na kuelekea kituo cha polisi, akaelekea moja kwa moja chumba cha mahojiano akamkuta Judith akiwa anamsubiria.
Kabla hajaanza na Judith, akaikuta baasha pale mezani, hapana shaka ilikua ikimsubira yeye. Alipofungua akakutana na ujumbe mwingine uliomkata maini yake, Naam! haraka akachomoka pale na kumuacha Judith akiwa kwenye uangalizi, akachukua gari yake ndogo na kuelekea Hospitali ambako maiti zilikua zimehifadhiwa.
Akaiomba maiti ya Sandra, ikaletwa kwenye chumba maalum kisha paja la Sandra likafunuliwa, akaiona Tatuu yenye jina la Bosco kisha akaifungua ile taarifa iliyopo kwenye baasha akagundua ufanano wa jambo fulani, pale pale simu yake ikaita. Akaweka miwani yake vizuri kisha akaipokea hiyo simu
“Zola! nafikiri umeupata Ujumbe wangu, Haraka sana anza na upelelezi wa kina…Hawa marehemu watatu huenda wakawa wanahusika na kifo cha Makam wa Rais” Ulikuwa ni ujumbe tata sana kwenye kichwa cha Inspekta Zola, jasho likawa linamtoka.
“Inawezekanaje? Wauwaji wakauwana wenyewe kwa wenyewe?” Akauliza Zola
“Zola, fanya upelelezi wako upesi. Idara yangu ya Usalama wa Taifa inakuamini sana ndio maana sijaona Mtu wa Kumpa hiyo kazi zaidi yako”.
“Oooops! sawa Mkuu” Akajibu kwa utiifu wa hali ya juu sana, Hofu ikatanda na hali ya tahadhari ikapanda kwenye kichwa cha Inspekta Zola, akajua sasa alikua kwenye kazi rahisi iliyogeuka kuwa ngumu kupita maelezo.
Kwenye Tatuu ya Jina ka Bosco kulikua na alama ya vidole viwili, alama hii ilikua maarufu sana miezi michache iliyopita baada ya kutokea kwa vifo vingi vya Watu wa Usalama, na viongozi wa juu wa Serikali, kila aliyeuawa alikutwa na muuli wa alama ile ya Vidole, hapo ndipo wasiwasi ulipoibuka baada ya kukutwa kwa Tatuu kwenye mwili wa Sandra.
Mara moja simu ya Inspekta Zola ikaanza kuita, ilikua ni simu kutoka kituo cha Polisi.
“Unasemaje?” akauliza Inspekta Zola akiwa amesimama kando ya maiti ya Sandra
“Nakuja haraka sana” akasema Zola kisha akachukua gari kurejea kituo cha Polisi, akasikia Milio ya gari za kubebea wagonjwa kutoka kituo cha polisi, maiti zilikua zimezagaa eneo la kituo cha polisi.
Zola hakuamini macho yake, Polisi mmoja akamfwata Zola na kumwambia kuwa yule Binti aliyekuwa akihojiwa ndani ya kituo hicho ndiye aliyekuwa amesababisha madhara yale
“Inawezekanaje binti dhahifu kama yule awashinde zaidi ya Askari 15 na kuwauwa wote?” Akauliza Zola huku akiwa anatazama jinsi maiti zilivyokuwa zikichukuliwa na kuwekwa kwenye Magari ya kubebea wagonjwa.
“Inspekta, Binti anaonekana kuwa na mafunzo ya kimapigano na ujasusi wa hali ya juu sana” Baada ya kusikia hivi Inspekta Zola akaelekea ndani ya kituo, damu zilikua zimetapakaa huku matundu ya risasi yakiwa kwenye miili ya askari waliokuwa tayari wameuawa.
“Amechukua baadhi ya nyaraka kwenye masanduku” akaongeza askari ambaye alikuwa akimfwata Inspekta Zola kwa nyuma, akaingia moja kwa moja hadi kwenye kile chumba cha mahojiano ambacho alimuacha yule Mdada aliyejitambulisha kama Judith, akaona kuna ujumbe juu ya meza, akaufungua ukiwa kwenye baasha akakutana na ujumbe ulioandikwa “KIVULI CHA UMAUTI” alafu alama ile ya vidole ikawa chini ya maneno hayo.
“Uuupsss” Akashusha pumzi kisha akaketi kwenye kiti na kuegemea ile meza
“Ngoma hii ni ngumu sana kuicheza” akajisemea kwa sauti kuu huku akitikisa kichwa chake.
- •••••••••••••••
Ndani ya Jengo moja refu zaidi katika Jiji hili, kulikuwa na jamaa mmoja aliyeitwa Six, alikua ameketi huku akivuta sigara yake, mwili wa Six ulikua na tatuu nyingi sana za rangi, simu yake ilikua bize sana akionekana kupokea na kutoa taarifa.
Mara akaingia Judith Mdada ambaye alikua kwenye kile kituo cha polisi, alionekana kuwa mwenye msongo wa mawazo. Akafikia kuketi kwenye sofa karibu na Six, Six akatikisa rasta zake
“Mbona uko juu juu sana?” Akauliza huku akizima sigara yake, akatoa moshi mwingi mdomoni
“It’s a bit Strange ( Inatisha kidogo )”
“Kumetokea nini?”
“Walinishtukia ikabidi nipambane kujiokoa pale”
“Oooh! Shit” Six akaongea kwa hasira sana, Mdada aliyejitambulisha kwa polisi kama Judith akavua sura ya bandia.
“Hawajafanikiwa kukufahamu?”
“Yes! hawajanifahamu”
“Ok! Malaika usiye na dhambi” akaongea huku akiwa anapokea nyaraka zilizoibwa ndani ya kituo cha polisi.
Nje kidogo ya Jiji hili, Inspekta Zola alikua akipokea kazi kamili ya kuwasaka waliokuwa wakifanya mauwaji ikiwemo kifo cha Makam wa Rais ambaye alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake na kuzua taharuki kubwa.
Mbele yake alikua amesimama Mtu mmoja mwenye umri sawa na wake, wote walikua Wazee wenye utaalam wa upelelezi, Mzee huyu alijulikana kama Dawson maarufu kama Google. Jina hili la utani alipewa sababu ya taarifa nyingi alizonazo ndani ya kichwa chake, licha ya Mzee Dawson kuwa Mtu wa Usalama wa Taifa pia alikua ana kitengo chake cha Siri alichokipa jina la MPA ambacho kilikua kikidili na masuala ya Upelelezi wa kesi kubwa kubwa ndani na nje ya Nchi.
Walifanana sana tabia zao, walikua walevi wa sigara na nyakati fulani walikua wakitumia pombe kali, ilikua ni kawaida kwao tangu wakiwa vijana kwani kazi waliyokua wakiifanya iliwafanya watumie akili nyingi ili kupambana na uharifu,
“Kuna kundi linaitwa MAFIA GANG, ni kundi maalum kwa ajili ya Ugaidi…Mkuu wa kundi hili anaitwa John Brain ni mzungu anayeishi Uskochi, Kazi yake ni kuratibu mauwaji. Amefanya kazi katika Nchi nyingi na sasa yupo hapa Nchini ndiye anayeratibu mauwaji ya viongozi kwa maslahi yake binafsi. Mwaka 2003 nchini Congo walifanya mauwaji mengi sana, nakuamini Zola ndio maana nataka ufanye upelelezi wa kina, ukomeshe kabisa kundi hili hapa Nchini” Yalikua ni maneno ya Mzee Dawson yalitoka na moshi wa sigara.
“Kila kitu kipo tayari kwa ajili yako Zola, unahitaji kuikomboa Nchi yako. Nakufahamu vizuri linapokuja suala la kesi tata” Akamaliza kwa kumtakia kila la Kheri kwenye jukumu lake zito la kuliondoa kundi la MAFIA GANG lakini kichwani bado alikua anauwaza ule mkasa wa akina Robert, akajiuliza waliingiaje huko na nini kilipelekea wauwane.
Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA PILI
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
16 Comments
Narudi tena kusoma hadithi baada ya kusoma riwaya ya MSALA aina hii ya stories ndo napenda mim
Kitu kitamu sana
Tambara kama hili nikipewa Scene nauwa sana yani sema ndo ivo hatuna nyenzo huku kwetu😁
Tam saaana hiiii
Imekaa poa sana
Naisi hii hii itakua kali kama…MSALA…maana ile ilikua kali kuliko zote👍
Mambo ni 🔥
Asante Mtunzi na Admin
More Love from Kenya ❤️
Aaha kubandika na kubandua
👍👍
Tamuuuu
https://whatsapp.com/channel/0029VarTsGt1t90TiJVyWi0J
Tunasubiri nyungine mkuu
SAWA sawaa
Tunaomba t mwendelezo Admin unatucheleweshea utamu
Tunaomba muendlezo admin adi tutasahau story sasa dah
Very nice