Ilipoishia “Kuna kundi linaitwa MAFIA GANG, ni kundi maalum kwa ajili ya Ugaidi…Mkuu wa kundi hili anaitwa John Brain ni mzungu anayeishi Uskochi, Kazi yake ni kuratibu mauwaji. Amefanya kazi katika Nchi nyingi na sasa yupo hapa Nchini ndiye anayeratibu mauwaji ya viongozi kwa maslahi yake binafsi. Mwaka 2003 nchini Congo walifanya mauwaji mengi sana, nakuamini Zola ndio maana nataka ufanye upelelezi wa kina, ukomeshe kabisa kundi hili hapa Nchini” Yalikua ni maneno ya Mzee Dawson yalitoka na moshi wa sigara.
“Kila kitu kipo tayari kwa ajili yako Zola, unahitaji kuikomboa Nchi yako. Nakufahamu vizuri linapokuja suala la kesi tata” Akamaliza kwa kumtakia kila la Kheri kwenye jukumu lake zito la kuliondoa kundi la MAFIA GANG lakini kichwani bado alikua anauwaza ule mkasa wa akina Robert, akajiuliza waliingiaje huko na nini kilipelekea? Endelea
SEHEMU YA PILI
“Oooh! Jesus!” Akasema Zola huku akilikodolea macho gari la kifahari la Mzee Dawson ambalo lilikua likitokomea, mkononi alikuwa ameshikilia bahasha nyeusi ambayo ilikua maalum kwa ajili ya kazi za siri, alijua ni vitu gani vitakuwepo kwenye Bahasha hiyo.
Safari ya Inspekta Zola ilimchukua masaa takribani matatu kufikia yalipo makazi yake ya siri ambayo alikua akiyatumia kwenye upelelezi kila alipopata kazi ngumu mbele yake alijificha kwenye makazi hayo ambayo aliyapa jina la HOME TOWN.
Lilikua ni jumba lililopo karibu na fukwe ya Bahari ya Hindi, alichagua eneo hili sababu lilikua tulivu sana, licha ya kuwa ni eneo ghali sana lakini alimudu gharama ambazo alikuwa akilipiwa na kitengo cha Siri cha Mzee Dawson ( MPA )
Akabandua karatasi zilizopo kwenye ubao maalum, kisha akabandika karatasi nyeupe akachora kwa kalamu na maandishi yakapata kusomeka kama MAFIA GANG akimaanisha ndio kwanza alikua akiingia kazini kwa ajili ya kupambana na kikosi hicho hatari cha Bwana John Brain.
Ilikua tayari usiku umeshaingia, akapiga simu kwa Waangalizi wa zile maiti Hospitali kuwa hazipaswi kutolewa hadi pale upelelezi utakapo kamilika, Hivyo familia zisubirie kwanza kabla ya maiti za akina Robert kupatikana kwa ajili ya mazishi, alikua na lengo lake ndani ya kichwa chake kilichojaa nywele za mvi, akakuna kidevu chake baada kuwa tayari ametoa maelekezo muhimu sana.
Inspekta Zola licha ya kuwa umri ulikua umeenda kidogo lakini alikua akipenda sana visichana vidogo vidogo, akaondoka kwenye makazi yale akaelekea Baa kwa ajili ya kupata mvinyo na kuangalia Mwanamke wa Kustarehe naye usiku huo.
Akaagiza White Wine huku akikodolea macho baadhi ya visichana vilivyokua ndani ya Baa hiyo, alipomaliza kunywa akawa ameshapata Msichana wa kustarehe naye usiku huo ambapo akaelekea Kwenye Hoteli moja iliyopo mita kadhaa kutoka kwenye makazi yake ya siri. Akastarehe naye kisha akamuondoa usiku huo huo, akabadili hoteli ambako alilala hadi asubuhi.
Aliamka na uchovu kiasi, akapata Kahawa kisha akaondoka hotelini hapo akaelekea Hospitali, akaagiza iletwe maiti ya Sandra. Akaanza sasa kuikagua rasmi kwa kutumia jicho lake kali la kijasusi, akiwa amevalia miwani yake ya macho akagundua jambo, akaagiza mkasi na kisu, akavalia gloves kwanza.
Akawaambia Watu wa Maabara waongeze mwanga wa taa, wakafanya hivyo. Akaona alama kwenye sura ya Sandra ambayo ilionesha kuwa sura ile haikuwa halisi. Akafwatisha ile alama kwa kisu ndipo akaona sura ikijivua. Wote waliokuwa ndani ya chumba cha Maabara wakaingiwa na ganzi, lilikua ni jambo lililo hitaji umakini wa hali ya juu zaidi.
Sura ilipovuka wakaikuta sura nyingine kabisa, pale pale akavua gloves akachukua simu na kupiga picha kisha akapiga simu kwenye kitengo cha siri cha Mzee Dawson ( MPA )
“Nahitaji wataalam wa Maabara haraka sana kwenye Hospitali ya ST. James karibu na chuo cha Biashara” Ilikua ni sauti yake iliyojaa umakini zaidi, haraka wale wataalam wakawa wamewasili hospitalini hapo
“Chunguzeni maiti mbili za Robert na Bosco, vueni sura zao za Bandia kisha mpige picha mnitumie” Akawaachia maagizo, Inspekta Zola akaondoka pale Hospitalini akiwa na jambo jipya ndani ya akili yake, sasa ndio akawa na mashaka juu ya wapi walipo Akina Robert wa ukweli na kwanini wale wajitoe muhanga kupoteza maisha yao?
“Kuna jambo limejificha sio bure” Akasema Inspekta Zola akiwa kwenye gari yake, alikua akielekea ofisini kwa Mzee Dawson ambaye ni mtaalam wa Taarifa kutoka usalama wa Taifa.
“Naam! Zola , kuna jipya umeligundua?” akauliza Mzee Dawson baada ya kukutana ana kwa ana na Inspekta Zola
“Dawson!! hili jambo lina mchakato wa hatari unaohitaji utulivu zaidi”
“Hilo ndilo nililotegemea kulisikia kutoka kwako Zola, hii sio kazi ya kitoto ndio maana nimeileta kwenye meza yako, umekutana na kazi nyingi za hatari na zote umefanikiwa, hili haliwezi kuwa jepesi pia”
“Maiti zile zina sura za Bandia, inaonesha kuna mwamvuli wa Kifo uliotumika hapa ili kupumbaza akili za kipelelezi”
“Una maana maiti sio halisi kwa sura tambuliwa?”
“Ndio, hii moja wapo” Akamuonesha sura iliyokutwa kwenye maiti iliyotambuliwa kama Sandra.
“Wauwaji ni Watu wenye akili kubwa sana na inaonesha ni wazoefu wa hii kazi Zola, unatakiwa kuwa makini sana endapo watakugundua hali itakua mbaya, unatakiwa upate sura ya Bandia ili kuficha uhalisia wako” Akasema Mzee Dawson akionesha kuanza kulitazama jambo hilo kwa jicho la tatu.
********
Ndani ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa, Six na yule Mdada aliyejitambulisha kwa Inspekta Zola kama Judith lakini huku alikua akiitwa Malaika walikua wakisubiria ugeni ndani ya Uwanja huu.
Malaika alikua kwenye sura yake halisi, akionekana kama mdada mwenye majivuno sana, shingo yake ilikua na tatuu ya maua ya rangi aina ya Rose, iliwabidi kukaa hapo kwa zaidi ya nusu saa. Punde wakapata kumuona Mtu waliyekuja kumpokea, alikua ni Mzungu mwenye kibegi kidogo.
Safari ya kutoka Uwanja wa ndege kuelekea kwenye makazi yao ya siri ilianza, Mzungu alipofika kwenye gari akavua sura bandia. Yes! huyu ndiye John Brain ambaye idara nyingi za Usalama Duniani zilikua zikimtafuta lakini ilikua ngumu sana kumnasa, licha ya kuwa yeye ndio Bosi wa kundi la MAFIA GANG lakini pia alikua akipokea oda kutoka kwa Mabosi wake ambao walikuwa wa siri sana.
“Umefanikisha kuchukua nyaraka?” akauliza John Brain huku akiwa anaiweka ile sura ndani ya begi lake dogo ambalo lilikua na sura nyingine za Bandia ambazo alikua akizitumia mara kwa mara ili kuficha utambulisho wake.
“Nimefanikisha lakini kuna Mpelelezi mmoja makini anafwatilia jambo hili”
“Dammn!! niliwaambia mnatakiwa kwanza kusafisha kikosi cha Usalama wa Taifa ndipo kazi nzito ianze” John Brain akachukua nyaraka na kuanza kuzipitia, alifahamu lugha zaidi ya 20 hivyo hakupata shida pindi alipokuwa akiratibu mpango fulani kwenye Nchi tofauti tofauti.
- ••••••••
Ndani ya Ikulu, Mzee Dawson alikua akifanya mazungumzo na Rais wa Nchi ili kujua wamefikia wapi. Ilikua ni lazima wadhibiti MAFIA GANG kabla haijaleta mpasuko na taharuki kwa Wananchi, tayari Watu ambao hawakua Usalama wa Taifa walianza kufa, vifo vya Askari 15 ndani ya kituo cha polisi ilikua ni miongoni mwa taarifa zilizomkasirisha sana Rais.
“Dawson! Unasifika kwa Ujasusi, tayari kazi hii iko mikononi mwako na hakuna namna tunaweza kufanya bali kusikiliza maendeleo yako” Yalikua ni maneno ya Rais, Mzee Dawson alikua akichezea karamu kuonesha alikua akitafakari namna ya kumjibu, Rais akagonga meza kama ishara ya kuhimiza kupata jibu kutoka kwa Mzee Dawson
“Kazi iko kwenye mikono yangu Mkuu, ni lazima nilifyeke kundi hili kabla halija leta madhara zaidi”
“Madhara zaidi? tayari wameleta madhara na hofu imetanda kwa watendaji wa Serikali, najiuliza ni Watu wa namna gani hawa wameweza kuingia kwenye nyumba ya Msaidizi wangu ( Makam wa Rais ) na kufanya mauwaji bila Askari na walinzi wengine kujua, hali sio shwari Dawson” Rais akapaza sauti iliyoambata na kukauka kwa koo lake, akahitaji maji ya Baridi kutoka kwenye friza, Dawson akampatia maji kwenye glasi, yalikua ni maongezi ya siri kati ya Dawson na Rais huyu. Baada ya kumaliza kunywa glasi moja ya maji baridi, akawa ametuliza mzuka wake.
“Dawson! nakuamini” akasema Rais akiwa anaweka glasi juu ya meza kisha akavuta tai yake
“Sitakuangusha Mkuu ni jukumu langu zito, nimekula kiapo kuilinda nchi yangu” akasema kwa utii na heshima kubwa mbele ya Rais huyu Kijana
“Wanataka nini?”
“Mapema tutalibaini hilo, kuanzia hapo tutawadhibiti Mkuu. Wamefanya mauwaji Nchi nyingi lakini hapa wameingia sehemu isiyo salama kwao, nakuhakikishia nitawafyeka haraka iwezekanavyo”
“Dawson! Nchi inakuangalia wewe na kitengo chako cha Usalama wa Taifa” Akamaliza kwa kumrunusu Dawson akaendelee na majukumu yake mazito, jasho likiwa linamvuja…Mzee Dawson akachukua Lifti kushuka chini, akaingia ndani ya gari yake.
Jua lilikua tamu sana siku hii, hali ya ubaridi ikiwa inachukua nafasi kubwa. Inspekta Zola akaelekea nyumbani kwa Marehemu Robert, Waombolezaji walikua wengi sana lakini Zola akahitaji kuonana na Mama yake na Robert, akaoneshwa mahali ambapo Mama huyo alikuwepo.
“Pole Mama, Naitwa Inspekta Zola nafikiri unanikumbuka?” akaongea baada ya kuketi, akahitaji kuzungumza na Mama yake Robert pekee, waombolezaji wengine wakaamriwa kutoka.
“Mara ya Mwisho ulionana wapi na Robert?” Mama akafuta chozi lake, akajiweka sawa kuongea
“Nilizungumza na Robert kupitia simu, akaniambia nije huku kwa ajili ya harusi yake. Nilichelewa kufika huku kutokana na mazingira yaliyo nje ya uwezo wangu, Alinisistiza sana natakiwa kuwepo lakini nilifika siku ya harusi…”
“Ulionana na Mwanao baada ya kufika?”
“Hapana, alipofika kanisani hakupata hata kunitazama. Ndio tukio likatokea…”
“Mwanao alikua anafanya kazi gani?”
“Robert alikua na duka la kuuza Maua mjini, ndio biashara yake ya muda mrefu”
“Unamfahamu vipi Bosco?” Mama akaanza kulia, Zola akajitahidi kumtuliza
“Bosco ni kama Mwanangu, walikuwa wakija pamoja kunitembelea, sijui wamepatwa na nini hadi wakauwana” Inspekta Zola alipomaliza kuzungumza na Mama Robert, akaelekea kuonana na Mzee Dawson ambaye alimpigia simu kuwa kuna ujumbe kutoka kwa Rais
Ndani ya mkoba wa Inspekta Zola kulikua na sura za bandia ambazo alikua amepewa na Mzee Dawson ili kuficha uhalisia wake, alipofika kwenye gari akaivaa kisha akaelekea kuonana na Dawson.
Kama kawaida yao walikutana sehemu iliyojificha huku wakipata pombe ambayo kwao waliita kama kifungua kinywa, sura ya Mzee Dawson ilikua imekosa neema ya furaha, tabasamu lake halikuonekana hata chembe na kumfanya Zola atamani kusikia kutoka kwa Mzee Dawson ( Google )
“Hali ni mbaya Zola, Mkuu amewaka sana leo anahitaji kazi iishe ndani ya muda mfupi vinginevyo anaweza akaajili Watu kutoka nje ya Nchi kwa ajili ya upelelezi wa kina kuhusu MAFIA GANG” akasema kwa sauti iliyotoka kwa vituo vituo huku akiwa anameza funda za pombe
“Dawson! umenipa kazi ndani ya masaa 24, ndani ya Upelelezi huu kuna visa tata sana ambavyo vinahitaji umakini wa hali ya juu sana vinginevyo tutakuja kupoteza kila kitu”
“Kuna Mtu nitakuunganisha naye, ni rafiki yangu wa muda mrefu anaitwa Pacho…atakusaidia baadhi ya mambo ili kuendana na muda”
Punde simu ya Mzee Dawson ikaanza kuita, akaisikilizia kwa miito mitatu kisha akaipokea na kuiweka kwenye sikio lake lililojaa Usikivu wa kupokea taarifa, alichokisikia kilimshtua sana mara simu ikakatika.
“Barabara namba 8 kuna mauwaji yametokea ya Afisa wa Usalama akiwa anatoka kanisani” Ilikua ni sauti ya Mzee Dawson iliyotawaliwa na utulivu sana
“Ooh God”
“Ndio hivyo Zola, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa wiki hii na kuendelea”
“Ngoja nielekee eneo la tukio” Inspekta Zola akajikusanya na kuondoka pale akimuacha Mzee Dawson akiendelea kugida pombe kali.
Yalikua ni majukumu yake ya kazi, akafika eneo la tukio na kuukuta mwili wa Afsa aliyeuwa ukiwa juu ya daraja, gari ya Afsa huyo ikiwa imesimama katikati ya Barabara na kusababisha msongamano.
Taratibu za kiusalama zikaanza mara moja huku mwili ukichukuliwa na kupelekwa Hospitalini, mara simu ya Zola ikaingia ujumbe kutoka kwa wataalam wa Maabara kutoka kwenye kitengo cha Siri cha Mzee Dawson kilichoitwa MPA, akapewa taarifa juu ya Maiti ya Robert na Bosco.
Milii ile ilikuwa ndio pekee yenye sura halisi tofauti na Maiti ya Sandra ambayo ilikutwa na sura bandia, akajikuta akiwa njia panda hajui aanze na lipi amalizie lipi, simu yake ikaingia ujumbe mfupi kutoka kwenye namba ambayo ilikuwa ya siri
“ZOLA TOKA ENEO HILO HARAKA SANA” Ujumbe ulisomeka hivyo, akajaribu kutafakari kwa kina lakini hakupata majibu kwa haraka, akajaribu kuujibu ujumbe huo lakini hakufanikiwa kupata majibu. Kwa akili yake ya kipelelezi akajuwa mara moja yupo Mtu anayemuona pale, haraka akaondoka pale na kuelekea kwenye gari lake ambalo lilikuwa kando na eneo lile, mara akasikia mlipuko mkubwa. Alipogeuka akaona gari moja ikiwa inawaka moto, ndio gari ambalo alikuwa karibu nalo pale alipokuwa amesimama eneo la tukio.
Hapo akafanikiwa kujua kuwa kuna Watu wanamfuatilia kwa karibu sana lakini akawa na maswali mengi kuwa ni nani aliyemuokoa kwenye ile hatari? Mlipuko ulisababisha majeruhi wengi sana ambao walikuwa ni Askari na wapita njia.
Alipofika kwenye gari yake akapata shahuku ya kutaka kumfahamu aliyemuokoa kwenye kifo, akachukua simu yake na kujaribu kuujibu ule ujumbe lakini hakupata majibu mengine, akamtafuta Mzee Dawson na kumtaarifu juu ya tukio hilo la mlipuko
“Aliyekuokoa anaitwa Pacho, ndiye msaidizi wako kwenye majukumu”
“Oooh! niliona kifo changu pale”
“Kuwa makini sana, Watu wa Usalama wanauawa sana….” yalikua ni maneno ya mwisho ya Mzee Dawson kisha simu ilikatika, ikampa wasaa Inspekta Zola kuelekea kwenye makazi yake ya Siri karibu na ufukwe.
Masaa mawili baadaye yalimkuta Inspekta Zola akiwa amekalia kiti kwenye makazi yake ya siri, mbele yake kulikuwa na meza nyeusi ngumu iliyotengenezwa kwa kioo. Alionekana kuzama kwenye lindi la mawazo, akafikiria namna Muuwaji alivyokuwa akifanya mauwaji kila kukicha, bado alitakiwa kujuwa ni wapi alipo Sandra wa Ukweli kama Bosco na Robert ni Watu halisi, presha ya Rais ya kulazikisha kazi ifanyike upesi ilimkasirisha sana.
*****************
Anga lilibadilika kuwa jeusi machoni pa Idara za usalama wa Taifa, Mauwaji ya Polisi na Maafisa yalitaarifiwa kila kona ya Jiji, Hofu ikachukua nafasi kubwa kila mmoja akijiuliza ni nani atafuata Kufa. Ujio wa John Brain Nchini ulikuwa na lengo moja kubwa, akakutana na Vijana wake wawili aliowatumainia sana mmoja aliyeitwa Six na mwingine aliyeitwa Malaika akawaambia
“Wakati Polisi wanahangaika kutafuta ufumbuzi wa vifo hivi vya utata sisi tutakuwa bize kumalizia mpango wetu hapa Nchini, Rais wa Nchi hii alitutuma kazi na tumeimaliza sasa kwanini idara yake inamshikilia Jamaal?” Alihoji John Brain
“Huyu Kenge anayeitwa Zola atakuwa kikwazo kikubwa sana kwenye mpango huu, lazima aondoke kwanza” Alisema Malaika akakumbuka jinsi Inspekta Zola alivyo makini
“Udhaifi wa Zola ni Wanawake, kilevi chake kitamuuwa muda mchache ujao” Alisema John Brain aliyeonekana kujaza mambo mengi kichwani pake
“Kazi hiyo niachieni mimi” Six akaomba apewe huo mpango wa kuondoa uhai wa Inspekta Zola
“Unatakiwa kuwa makini sana sababu kwa namna alivyo huyo Mtu si rahisi akamuamini Mtu kwa Mara ya kwanza, unapaswa pia kujuwa kuwa ukibainika basi kila kitu kitaharibika. Zola ni Jasusi mbobezi, kabla hujampeleleza anakuwa tayari amekupeleleza.” Alisema John Brain, kisha Malaika kasema
“Zola anatumika kama Mwanvuli wa Serikali katika kutekeleza mipango ya siri, najiuliza aliwezaje kukwepa mtego wa Bomu”
Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA TATU USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
7 Comments
First one
Huna Baya Mwanangu
✌️✌️
Waaah😋
Doooh mambo mengi kwel
Imekaa poa sana
♥️