Ilipoishia “Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua bangi yangu? Sikujibiwa na mtu, ukimya ulitawala huku akili ikiniambia wale wapangaji wenzangu watakuwa wanahusika moja kwa moja.
Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda chumbani. Nilifungua mlango na kusimama kwanza kabla ya kuzama ndani. Niliangaza kila kona, nikabaini kitu. ”
Tuendelee SEHEMU YA 07
Niligundua kwamba, kuna mtu alikaa kitandani maana nilipoondoka asubuhi nilikuwa nimekitandika, muda huo kwa pembeni upande wa mbele kulikuwa na alama za makalio.
Alama hiyo ilinipa picha kuwa, aliyekaa alikuwa na makalio makubwa sana! Nilipoangalia chini kwenye kapeti nikabini kitu kingine kwamba, aliyekaa alikuwa na mafuta kwenye miguu kwani iliweka alama kuzunguka miguu yake.
Aidha, nilibaini jambo jingine kwamba, aliyekaa kitandani pia alikuwa akisimama na kutembeatembea kwani alama ya miguu yenye mafuta ilionekana sehemu mbalimbali za chumbani kwangu.
Mara nikasikia hodi ikigongwa mlango mkubwa. Niliikumbuka ile sauti kwamba ilikuwa ya yule msukuma mkokoteni wa maji.
“Nakuja,” nilisema kwa sauti kupitia dirishani kwani chumba changu na sebule yangu vilikuwa upande wa mlango mkubwa wa kuingilia.
Nilitoka mpaka mlangoni, nikafungua na kumkuta yule kijana.
“Bro vipi, wapo wale watu ndiyo nimekuja hivi.”
Nilimshika mkono, nikamvuta kumwingiza ndani bila kusema naye. Nilimwelekeza vyumba vya wale wapangaji wenzangu kisha mimi nikaingia chumbani kwangu.
Nilikaa kitandani na kutega sikio kitakachotokea huko. Nilimsikia yule kijana akigonga mlango. Aligonga mara tatu, kisha nikasikia mlango ukifunguliwa, sikuamini. Nilitaka kutoka, lakini nikasema nisubiri hadi mwisho nione.
Baada ya mlio wa kufunguliwa kwa mlango, ukafuatia mlio wa kufungwa halafu ukapita ukimya. Akilini nilijua wamemkaribisha na wakafunga mlango na sasa wanaongea naye.
Cha ajabu, kila nilipofuatilia ili kujua kama mlango utafunguliwa na yule kijana kutoka, sikufanikiwa kugundua hali hiyo, nikaanza kupata wasiwasi.
“Inamaana tangu wakati ule hadi sasa bado wapo ndani? Wanaongea nini sasa? Au wanapigiana mahesabu? Si yule kijana alisema anadai pesa nyingi?” maswali hayo yote yalikuwa yangu lakini majibu yake sikuyajua.
Usiku uliingia, muda ukazidi kwenda, sikusikia ishara yoyote ya yule kijana kutoka. Zaidi sana nilisikia wale wapangaji wenzangu wakipika kwa kukaangiza kitu kama nyama.
Usiku nilitoka, nikaenda kutafuta chakula, nikarudi nacho nyumbani. Nikala, nikaenda kuoga, nikarudi kitandani na kulala, sikuona dalili ya mawengewenge wala mang’amng’amu.
Asubuhi niliamka kwa kushtuka, lakini sijui nini kilinishtua ila ni kama kuna mtu alinishika mguu. Hakukuwa na kitu chochote chumbani mwangu. Nilitoka na kwenda kusimama kwenye dirisha, nikachungulia nje. Kulikuwa shwari.
Nilipotoka kuoga nikiwa navaa nguo ili kuondoka, nikasikia wenzangu wakitoka. Nilisimama tena dirishani kwani kwa mtu anayetoka kwenye nyumba ile na kwenda popote ilikuwa lazima apite mbele ya dirisha langu.
Baada ya muda walifungua mlango mkubwa, nikasikia wakiufunga, lakini baada ya hapo sikumwona mtu yeyote yule akipita mbele ya dirisha.
Na mimi nilipomaliza kujiandaa, nilitoka, nikafungua mlango na kutoka. Mbele kidogo nilikutana na watu kama kumi wamesimama wakiongea. Niliwasalimia nikawauliza kama kuna usalama.
“Usalama ni mdogo bwana, kuna kijana mmoja amepotea. Tangu jana usiku alipotoka kwa mkewe akasema anafuatilia madeni ya biashara zake hajarudi,” alisema mzee mmoja ambaye alisimama akiwa amejishika mikono kwa nyuma.
“Ni biashara gani anafanya?” niliuliza.
“Huwa anauza maji kwenye mkokoteni.”
“Ha! Ni yule muuza maji?”
“Huyohuyo,” alisema yule mzee.
Akili za haraka nikasema hapa ndipo pa kujua wale wapangaji ni akina nani, inabidi niseme ukweli ili waende polisi, najua polisi watakuja kukagua ndani.
“Lakini mbona jana usiku alikuja kwangu kudai pesa yake?” nilihoji kwa uso wa wasiwasi.
“Ulipomlipa akaondoka?” mwanamke mmoja aliniuliza.
“Siyo kwangu, ila mimi ndiye niliyemfungulia mlango. Alipoingia akawaulizia wapangaji wenzangu, nikawaonesha chumba, akapiga hodi, akakaribishwa ndani.”
“Hukumuona kutoka?”
“Kwa kweli sikufuatilia maana na mimi nilirudi chumbani kwangu.”
Wale watu wakaniuliza kama naweza kuwapeleka pale nyumbani, nikawaambia kwa muda ule hapakuwa na mtu nyumbani, wanarudi jioni.
“Basi tunakwenda kuwaambia ndugu zake, jioni watakuja, si nyumba ile pale?”
“Ndiyo.”
Nilipofika kazini na kuanza kazi, akili zangu zikawa zimefunguka kitu. Nilijiambia wale watu wakijua ni mimi niliyetoa mchoro wote, watanifanyaje?
Nilibaini nimechemsha, lakini nikasema moyoni kwamba potelea mbali, wajue wasijue sawa tu.
Kuna wakati nilipigiwa simu, namba sikuitambua, yaani ilikuwa ngeni kwenye kumbukumbu zangu. Nilijiuliza mwenyewe kwamba anaweza kuwa nani, lakini sikupata jibu.
Awali nilisita kuipokea kiasi kwamba ilikata, mpigaji akapiga tena. Nikaamua kuipokea sasa:
“Halooo,” nilivuta sauti.
“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana,” alisema huyo mtu bila kujitambulisha kisha akataka simu.
Nilishangaa sana, nikaanza kazi ya kuwaza kwamba anaweza kuwa nani na ni kwa nini aniambie angalia sana?
“Atakuwa jamaa wa nyumbani, kwa vyovyote vile,” nilisema moyoni na kuamini hivyo kwani kwa maisha ninayoishi mimi si rahisi kuwa na maadui. Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa wasiwasi. Nilijua nimeingia kwenye mapambano makubwa na wale wapangaji wenzangu.
Niliendelea kufanya kazi, lakini sikuwa na amani tena. Mara alitokea yule mfanyakazi mwenzangu ambaye alinipa ushauri wa kupulizia bangi ndani ya nyumba ili kuwakimbiza majini au viumbe wote wabaya.
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?” nilimuuliza huku nikiwa namtazama. Kisa cha kumtazama kwanza ilikuwa kujiridhisha kama kweli ni yeye au wale wapangaji wenzangu wameamua kunifuata ‘laivu’.
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilipomkazia macho sana, akasema ana kazi nyingi, akageuza na kuondoka. Mlango ulipojifunga tu, nikajiegemeza kwenye meza na kuwaza mambo kibao. Ilikuwa kama nataka kusinzia, lakini nikasikia sauti kichwani zikisemezana hivi:
“Halooo.”
“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana.”
Mara nikasikia tena zikisemazana hivi:
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?”
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilishtuka na kusimama, nikaondoka kwenda nje. Nilikutana na yule mfanyakazi tena, akaniuliza kama naondoka.
“Vipi, unaondoka saa hizi?”
“Bado nipo.”
“Kwanza nilisahau kukuuliza, vipi ulifanikisha ile kitu ya kuvuta kama nilivyokwambia?”
Moyo ulishtuka, nilijua ni watu wawili kwani huyu angekuwa yule aliyenifuata muda ule, asingesema alisahau kuniuliza.
“Nilifanikiwa kupata bwana, lakini,” nilisema nikimshika mkono, nikamvutia pembeni kidogo.
“Kaka mambo makubwa kule. Kwanza unajua kama nimekuona wewe mara ya pili hii leo?”
“Kivipi?” aliniuliza.
Nilianza kumsimulia kila kitu, kuanzia zile bangi hadi nusu saa kabla sijaonana naye. Alishangaa sana, akasema yeye ndiyo kwanza anaingia, alikuwa Kariakoo, pia akasema kwa siku hiyo ndiyo kwanza ameniona mimi muda ule.
“Sasa itakuwaje ndugu yangu?” aliniuliza.
“Sielewi.”
“Sasa sikia, mimi ninajua nitapata wapi bangi, we usiku saa moja niambie tukutane wapi, nitakuja nayo halafu nitaiwasha na kuivuta mimi.”
“Wewe huogopi?”
“Niogope nini?”
“Kufa.”
“Nani ataniua?”
“Si hao watu wabaya.”
“Hamna, hawawezi.”
Nilimkubalia, nikamwambia nitampigia saa moja ili tukutane akiwa na hiyo bangi yake.
Akili zangu hazikukaa sawa, niliondoka kwenda kutafuta maji ya kunywa, kisha nikaenda kupumzika kwenye kibanda cha kuuza vocha za simu.
Pale, mtu yeyote anayenijua angeniona angebaini nina matatizo mazito kichwani mwangu, kwani sikuwa sawa hata usoni. Muda mwingi niliwaza maisha ya kwenye ile nyumba, hasa usiku wa siku hiyo ambapo najua wale watu wakija ndiyo balaa litakuwa kubwa zaidi.
“Halafu usiku wa leo lazima watakuja kunifanyia maajabu yao, lakini dawa yao nisilale. Oke, kumbe bangi itapulizwa leo, kidogo itakuwa nafuu,” nilisema moyoni, nikashtuliwa na sauti ya kike nyuma yangu iliyoita jina langu.
NILIPOGEUKA nyuma, nikamwona dada mmoja aitwaye Mwantumu Seleman nilikuwa naishi naye Mwananyamala. Akaniuliza habari za siku. Niliamua kumsimulia janga langu, lakini ghafla likaja gari, akaingia huku akiniambia atanitafuta siku nyingine.
Baadaye nilirudi kazini huku nikiwa na hali ya wasiwasi, hata kazi zangu zikuzifanya sawasawa kama ilivyo kawaida yangu. Iliniuma sana!
Muda wa kazi ulipokwisha, niliondoka moja kwa moja hadi nyumbani. Sikutaka kupitia mahali siku hiyo, lakini nilishakubaliana na yule mfanyakazi mwenzangu aliyesema atakuja na bangi yake.
Wakati nafungua mlango mkubwa nilibaini wenzangu walisharudi maana mlango haukufungwa na funguo, nikaingia ndani. Nilipofika kwenye mlango wangu wa kuingilia sebuleni, wakati naufungua nikasikia mlango wa chooni unafunguliwa, yaani kumaanisha kwamba kuna mtu anatoka.
Ukisimama mlangoni pangu, mtu akitoka chooni unamuona bila kificho, hususan kama anakuja vyumbani. Lakini pia hata akiwa anatoka kwenda uani, utamuona kwa mgongoni. Nilisita kuingia nikiamini nitamwona mtu huyo. Nilianza kuona miguu ikitoka, moyo wangu ukashtuka, mara nikamwona mtu mwenyewe.
Nilijikuta nikisisimka mwili, niliamini naona kivuli chake na si yeye. Ni mtu mweusi, wakati nilitarajia angekuwa mweupe.
Alivyozidi kunisogelea, nikabaini kuwa, ni yule kijana muuza maji kwenye mkokoteni.
“Ha! Wewe vipi, unatafutwa sana unajua?” nilimwambia.
Badala ya kunijibu, alikata kona kuufuata mlango mkubwa. Na mimi nikamfuata kwa nyuma, nilimkuta akiwa anamalizikia kutoka nje. Niliitupa simu kwenye kochi kisha nikatoka kumfuata, na mimi nilifungua mlango ambao ulishaanza kurudi baada ya yule kijana kutoka.
Nilishangaa kutomuona popote kule nje. Wazee wawili walikuwa wanapita, nikawauliza kama wamemuona mtu ametokea mlangoni pale, wakasema hapana, ila kuna mbwa alitokea ndani kazunguka nyumba.
“Mh! Mbwa tena?” niliwauliza wale wazee, nao wakasisitiza kuwa ni mbwa, tena mweusi.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio, wasiwasi uliongezeka kiasi cha kunifanya niishiwe nguvu. Wakati huo wale wazee walikuwa wakimalizikia kwa mbali. Niliogopa kurudi ndani, nikawa nimesimama mlangoni.
Wazo lilinijia kwamba, nimpigie simu yule mfanyakazi mwenzangu kumuomba aje mapema maana hali ni mbaya sana. Lakini simu nayo ilikuwa sebuleni kwenye kochi, nitaipataje, yaani nitaifuataje kule ndani wakati niliamini tayari kumeshakuwa ukanda wa kifo?
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla kwenye dirisha la chumbani kwangu nikaona kama mtu anachungulia nje, nilikaza macho ili kumwangalia vizuri, akapotea.
“Mh! ni kweli?” nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni kwamba alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme Mwafrika kama mimi.
Nilikwenda pale dirishani, nikapanda ili kuchungulia, nikaona mlango unafunguka kuashiria kuna mtu alitoka maana mlango ule ulikuwa hauwezi kukaa wazi, ni lazima ujifunge wenyewe na mbaya zaidi mimi nilikuwa sijaufungua zaidi ya ule wa sebuleni.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anakuja kutokea upande ninaoondokea kwenda kazini, simfahamu lakini nilimsimamisha.
“Bro kuna ishu hapa inatisha kidogo, naomba msaada wako.”
“Kuna nini?” aliniuliza.
Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini, sikugusia mambo ya nyuma.
“Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?”
“Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue simu yangu tu nimpigie huyo jamaa.”
“Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina haraka sana leo,” alijitetea yule mtu ambaye kwa umbo ni bonge la mtu. Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala kuchelewa. Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu ya 08
Tafadhali Unapomaliza Kusoma Acha Na Comment Yako Hapo Chini
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
Una Enjoy Nyumba Ya Majini? Mtumie ADMIN Ahsante
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.
Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz
26 Comments
Mmmhhhh mambo ni motoo
hadithi ipo🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥
🔥
🥹😭🤔🤔Atari na nusu🙌🙌
Magomeni mwembechai iyo sio poa nimesoma makurumla naelewa
Aah hii ya leo 🔥🔥🔥
Hatarii
😁😅😆🤣😂😀
Inatisha na kuogopesha
Na hali inavyoonekana kijana mpangaji kila atakayekutana naye atahisi ni jini
😀😀
Nimesikitika😓
Maua yako admin
Nmeogopaa🥺
😂😂🥲🥲🥲💔sipangi mimi mwenyew sku zote ntakaa na mamangu🥲🥲🥲 khaaaa mwandishiii ishia apo apo naogopaaa😭😭😭💔
Admin uwe unazituma mbili mbili kwa siku…maana ni moto
Daaahhh admni mbna watufanyia hivyo achia mbilimbil
Appreciate bro ya Leo ni moto🔥🔥
🔥🔥 🔥
🎉🙌
Hahahaaaa
🔥 🔥 🔥 Hatariiii na nusu
Mwandishi nmesoma stori huu usiku naogopa kulala😫😫😫😫😫
Story nzuri admin tumpe maua yake * kijiweni forever*
Aaah tangu nilivyo onajinalake ya k1 sijawah soma usiku🥺 nasitoisoma usiku…
Alafu adnin vipande ni kidog sana
Daaah ni nomaaaa!!
duuh balaa duniani mi naacha kila kitu nakula kona
Umetisha
Hii ni balaa